*HEROIN
Ni aina ya dawa ya kulevya
inayotengenezwa na kemikali ya asili inayoitwa ‘morphine’ ambayo inapatikana
kwenye utomvu ‘opium’ wa tunda la mmea wa afyuni ‘opium poppy’ unaolimwa zaidi
kwenye nchi za Afghanstan, Myanmar na Laos. Hapa nchini, heroin inashika nafasi
ya pili kwa matumizi baada ya bangi, na inatumiwa kwa njia ya kuvuta ikiwa
imechanganywa na kiasi kidogo cha bangi na sigara au kwa njia ya kunusa na
kujidunga. Heroin ni kati ya dawa za kulevya zinazoongoza kwa kusababisha uteja
haraka, vifo vinavyotokana na kuzidisha kiasi cha matumizi au maradhi
mbalimbali, pia ni dawa ambayo ina watumiaji wengi wanaohitaji tiba. Heroin
hujulikana kwa majina ya mtaani kama unga, ngada, teli (cocktail), msharafu,
white, kijiwe, brown, nk.
Utomvu ukivunwa kwenye mmea wa afyuni
(opium)

MADHARA YA HEROIN
Kiafya
- Husababisha
magonjwa ya moyo, ini, mapafu, meno, ngozi, figo na saratani
- Mazingira
duni ya utumiaji na kushirikiana vifaa husababisha maambukizi ya kifua
kikuu, VVU na homa ya ini
- Matumizi
ya heroin na pombe huweza kusababisha kifo
- Mtumiaji
anapoacha kutumia heroin hupatwa na arosto inayoambatana na dalili
zifuatazo maumivu makali, homa, kuharisha, kizunguzungu na kichefuchefu
- Heroin
hupunguza kasi ya utendaji kazi wa mfumo wa fahamu na kuathiri umakini, hivyo
kusababisha ajali au kushiriki ngono zembe.
- Kukosa
hamu ya kula na kudhoofu kiafya
- Upungufu
wa maji mwilini kunakosabisha kukosa choo
- Kujidunga
husababisha mishipa ya damu kusinyaa au kupotea na hivyo kushindwa kupata
msaada wa matibabu kwa haraka inapohitajika
- Huweza
kusababisha vifo kutokana na kuzidisha kiasi cha matumizi
Kijamii
- Mtumiaji
kutowajibika na kushindwa kutimiza majukumu katika familia na kusababisha
kuvunjika kwa ndoa, kutelekeza watoto na kwa watoto hufukuzwa na kuishi
kwenye mageto
- Ongezeko
la vitendo vya uhalifu vikiwemo udokozi, unyang’anyi, utapeli pamoja na
mmomonyoko wa maadili (biashara ya ngono).
- Biashara
ya heroin imesababisha vijana wa kitanzania kuwekwa rehani nje ya nchi
(bondi) na kuhatarisha maisha yao na taswira ya nchi.
- Biashara
ya dawa za kulevya huambatana na uhalifu mkubwa kwenye jamiikama ujangili,
biashara ya binadamu, biashara haramu ya silaha, money laundering,
utekaji, ugaidi, madanguro, nk
-
Kiuchumi
- Matumizi
ya dawa za kulevya hupunguza nguvu kazi ya taifa na kuongeza umasikini kwa
familia na jamii kwa ujumla.
- Biashara
ya dawa za kulevya husababisha mzunguko wa fedha haramu, mfumuko wa bei,
utakatishaji fedha, kukithiri kwa rushwa na kuongeza tofauti ya kipato
- Serikali
hutumia gharama kubwa kudhibiti tatizo la dawa za kulevya kwenye
ukamataji, matibabu, kutoa elimu, nk
Kwa wanawake
- Huweza
kuharibu mimba au kuzaa watoto njiti.
- Huzaa
watoto wenye uteja na heroin
- Watoto
wanaozaliwa hudumaa kimwili na kiakili na mara nyingi hufariki kabla ya
kufikisha umri wa miaka mitano
Wanafunzi
Wengi wanaotumia heroin hushindwa
kuzingatia masomo yao na wengine kushindwa kumaliza shule. Vijana hawa hujikuta
hawakubaliki katika jamii zao na kunyanyapaliwa hivyo hujiunga na magenge ya
wahalifu.

Utamsaidiaje mtumiaji wa heroin?
Mtumiaji anaweza kupunguza kiasi
anachotumia taratibu na hatimaye kuacha.Wanaweza kupatiwa tiba ya methadone
inayopatikana kwenye baadhi ya vituo vya afya. Aidha, asasi za kiraia
huwasaidia watumiaji kuacha kwa kuwapa unasihi na huduma nyingine. Vilevile,
nyumba za upataji nafuu ‘sober house’ huwasaidia kwa kuwapitisha kwenye hatua
12 za upataji nafuu.
Ujumbe kwa jamii
1. Wazazi na walezi wawalee watoto katika
maadili mema ikiwemo kuwa nao karibu na kuwasikiliza
2. Vijana wajitambue na kujiepusha na
makundi hatarishi yanayoweza kuwaingiza kwenye utumiaji wa sigara, ugoro,
pombe, shisha au bangi ambavyo watumiaji wengi wa heroin wanakiri walianza
navyo.
3. Usijaribu kuonja heroin kwani inaleta
uraibu (uteja) kwa haraka na ni vigumu sana kuachana nayo.
4. Watumiaji wasinyanyapaliwe waelekezwe
kwenye tiba